Monday, June 13, 2011

Askofu mkuu Anglikana atakiwa kizimbani

SAKATA la mgogoro wa Kanisa la
Anglikana mkoani hapa
limechukua sura mpya baada ya
Mahakama Kuu Kanda ya Arusha
kutoa hati ya kukamatwa kwa
Askofu Mkuu wa Kanisa hilo
nchini.
Mbali ya hilo pia Mahakama hiyo
awali ilisimamisha shughuli zote
za usimikaji wa Askofu na juzi
pia kutoa hati ya kukamatwa
kwa Askofu aliyesimikwa juzi,
Stanley Hotay.
Kutokana na amri hiyo, iwapo
Askofu Hotay atakamatwa na
kutiwa hatiani kwa kosa la
kukaidi amri ya Mahakama,
huenda akawa amepoteza sifa za
kuwania tena kiti hicho cha
uaskofu kwa mujibu wa taratibu
za kanisa hilo.
Kutolewa kwa hati hiyo na Jaji
Kakusulo Sambo kumekuja siku
moja baada ya juzi Askofu Hotay
kusimikwa kuwa Askofu wa
Kanisa la Anglikana Tanzania
badala ya Dayosisi ya Mount
Kilimanjaro.
Juni 10, Mahakama Kuu hiyo
ilitoa amri ya kuzuia kuapishwa
kwa Askofu Hotay, hadi shauri la
kupinga kusimikwa kwake
lililofunguliwa na waumini
watatu wa Kanisa la St. James
jijini hapa litakaposikilizwa na
kutolewa uamuzi.
Waumini waliofungua kesi hiyo
ni pamoja na Godfrey Mhone
ambaye ni mume wa
mwanamuziki wa injili nchini,
Beatrice Mhone, Lothi Oilevo na
Frank Jacob, ambapo kwa
pamoja wanadai kwamba
uchaguzi uliomweka madarakani
Askofu huyo una mpango
mahsusi wa kukiuka Katiba ya
Kanisa hilo.
Akitoa uamuzi wa Mahakama
hiyo mara baada ya kusikiliza
hoja za pande mbili katika shauri
hilo, Jaji Sambo alisema
ameridhika pasipo shaka
kwamba amri ya Mahakama
aliyoitoa Ijumaa ilipuuzwa.
Alisema katika kosa kama hilo,
sheria iko wazi kushughulikia
watu wanaokiuka amri za
Mahakama.
Alisema kwa vile shauri hilo
lilikuwa halimhusu Dk. Mokiwa,
lakini katika hatua nyingine
tayari amefanya jambo ambalo
limesababisha amri ya Mahakama
isiheshimiwe, “sasa natoa amri
ya Mahakama ya kumtaka Askofu
Mokiwa na Askofu Hotay
wakamatwe haraka sana. Na
uamuzi mdogo wa shauri hili
nitautoa baadaye.
“Kwa sababu huyu tayari
amekwishakuwa Askofu na mtu
akishasimikwa kuwa Askofu ni
kazi kweli kweli kumwondoa,”
alisema Jaji Sambu.
Huku akionekana kuwa mkali, Jaji
Sambu alisema pamoja na
Mahakama hiyo kutoa amri hiyo,
lakini kwa sasa itabidi kuangalia
upya tena namna ya kuendesha
shauri hilo kutokana na
kuapishwa kwa Askofu huyo.
Alisema kabla ya Mahakama
kusikiliza upande wa pili
uliokuwa unalalamikiwa, tayari
ulishamsimika Askofu Hotay
ambapo kwa hatua hiyo, ni sawa
na kupindisha utaratibu wa kesi.
Uamuzi wa kukamatwa kwa
maaskofu hao, ulitolewa baada
ya wakili wa upande wa
mashitaka, Meinrad D’souza,
kuwasilisha maombi maalumu
mahakamani hapo ili itoe adhabu
kwa Dk Mokiwa na Hotay,
kutokana na kukiukwa amri ya
Mahakama.
Akisoma uamuzi kwa Kiswahili
kwa takriban saa moja huku
akisikilizwa kwa utulivu na
mamia ya waumini wa Kanisa la
Anglikana waliofurika
mahakamani, hapo, Jaji Sambo
alisema haihitaji elimu ya chuo
kikuu kuona kuwa
walichokifanya maaskofu hao wa
Anglikana kuwa ni kudharau
amri halali ya Mahakama.
Awali wakili D’Souza alisema
kitendo cha Askofu Mokiwa
kumsimika Hotay kimeingilia
uhuru wa Mahakama na
kushusha heshma ya Mahakama
Kuu, kwani ilikishatoa agizo la
kusitishwa kwa shughuli zozote
za kuapishwa Hotay.
D’Souza alisema alichokifanya
Askofu Mokiwa juzi ni kuvuruga
mwenendo mzima wa kesi hiyo,
ambayo inapinga mshitakiwa wa
pili, Hotay kuapishwa kwani umri
wake umegushiwa, na Katiba ya
Anglikana inaeleza wazi kuwa
Askofu anapaswa kuwa na umri
unaoanzia miaka 40 lakini Hotay
ana miaka 38 na hivyo tararibu
zote za uchaguzi zilikiukwa.
Hata hivyo, mawakili wa upande
wa Utetezi, Joseph Thadayo na
Issa Mavura, waliiomba
Mahakama itupilie mbali maombi
ya kuchukuliwa hatua maskofu
Mokiwa na Hotay kwa maelezo
kuwa hawakuingilia mwenendo
wa kesi hiyo.
Thadayo alimkabidhi Jaji Sambo
tamko la Askofu Mokiwa ambalo
linaeleza kilichotokea, kuwa
Hotay alisimikwa kama Askofu
wa Kanisa Anglikana Tanzania si
wa Dayosisi ya Mount
Kilimanjaro.
Mara baada ya uamuzi huo,
Wakili Thadayo alisema ni wa
Mahakama na hivyo hawana
jambo la kufanya zaidi ya
kutekeleza maagizo hayo.

No comments:

Post a Comment