Monday, July 25, 2011

Kikwete apunguza msafara wake

RAIS Jakaya Kikwete ameridhia
idadi ya maofisa katika ziara zake
za nje ipunguzwe ikiwa ni hatua
ya kupunguza gharama.
Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa,
Bernard Membe aliliambia Bunge
mwishoni mwa wiki wakati
akijibu hoja ya kambi ya upinzani
iliyoendelea kutaka safari za nje
kwa viongozi zipunguzwe.
Membe alisema katika safari ya
hivi karibuni ya Rais Kikwete
nchini Shelisheli, idadi ya maofisa
alioongozana nao ilikuwa 34 na
kwa safari ya Afrika Kusini
ilikuwa 34.
Hata hivyo, Waziri Membe alisema
wakati mwingine, wingi wa
maofisa huzingatia na aina ya
ziara na nchi anakokwenda.
Alitoa mfano kwamba, endapo
anakwenda nchi ambayo ulinzi
wake upo shakani, idadi inaweza
kuongezeka.
Alisema, zipo ziara nyingine
kama vile za kibiashara
inawezekana akalazimika
kuongozana na ujumbe wa
wafanyabiashara.
Awali, katika kuchangia hotuba
ya makadirio ya Mapato na
Matumizi ya Wizara
yaliyopitishwa, kambi hiyo ya
Upinzani kupitia kwa Waziri
Kivuli wa Wizara ya Mambo ya Nje
na Ushirikiano wa Kimataifa,
Ezekia Wenje ilisema safari za
viongozi wa juu zinatakiwa
ziendane na hali ya uchumi.
Wenje alisema katika dhana ya
kupunguza matumizi, baadhi ya
safari za nje ambazo siyo lazima
mkuu wa nchi kwenda, awaachie
viongozi wengine washiriki kwa
kuwa msafara wa Rais nje ya
nchi una gharama kubwa
ikilinganishwa na mawaziri au
maofisa wengine wa Serikali.
“Kambi ya Upinzani inaitaka
wizara ikishirikiana na ofisi ya
Rais kuweka utaratibu wa safari
za viongozi nje ya nchi, ili
kupunguza matumizi makubwa
ya Serikali na hatimaye fedha
hizo zielekezwe katika miradi
mbalimbali ya maendeleo,”
alisema Wenje.
Hata hivyo, Serikali imekuwa
ikisisitiza kwamba safari za Rais
Kikwete nje ya nchi ni zenye
manufaa na imekuwa ikitoa
mafanikio ya ziara hizo katika
nchi mbalimbali duniani.
Kwa mfano, Marekani ambako
Rais Kikwete amekuwa na ziara
tangu wakati wa utawala wa
Rais George W. Bush na sasa Rais
Barack Obama, Tanzania
imenufaika kwa kupatiwa fedha
nyingi katika miradi ya barabara,
umeme, afya na maji.

No comments:

Post a Comment