Tuesday, July 12, 2011

TANESCO YAELEZA KILICHOSABABISHA UMEME KUKATIKA UWANJA WA TAIFA

SHIRIKA la Umeme Tanzania
(Tanesco), limesema hitilafu za
kiufundi zilisababisha kutokea
kwa hitilafu ya umeme juzi katika
sehemu kubwa nchini na
kusababisha mikoa kadhaa kuwa
gizani kwa takriban saa tano.
Aidha, Tanesco imesema kituo
cha kupokea, kupoza na
kusambaza umeme cha Ilala, Dar
es Salaam kilipata hitilafu na
hatimaye kusababisha
kukosekana kwa umeme kwenye
Uwanja wa Taifa, wakati wa
fainali ya Kombe la Kagame kati
ya Yanga na Simba.
Meneja Uhusiano wa Tanesco,
Badra Masoud alisema hayo jana
katika taarifa yake kwa vyombo
vya habari na kueleza kuwa
hitilafu hiyo ilianza kujitokeza saa
12:53 jioni baada ya kituo cha
kupokea, kupoza na kusambaza
umeme cha Ilala kupata hitilafu.
Alisema, kutokana na hitilafu hiyo
maeneo ya Kurasini, Kigamboni,
Mbagala, Mkuranga na Uwanja
wa Taifa yalikosa umeme.
Alisema, mafundi wa shirika hilo
walitatua tatizo hilo ambapo
waliwaunganisha wateja wa
Uwanja wa Taifa kutokea katika
kituo kingine kilichopo Kurasini,
na umeme ulirejea uwanjani saa
1:20 usiku.
Hata hivyo, alisema baadaye
umeme ulikatika tena kutokana
na kukatika kwa Gridi ya Taifa
kutokana na sababu za kiufundi
zilizosababishwa na kukatika
kwa kiunganishi cha laini
iliyokuwa ikitokea katika kituo
cha kuzalisha umeme cha New
Pangani na kusababisha gridi
yote kuzimika hadi kupelekea
mikoa yote iliyoungwa nayo
kukosa umeme.
Alisema, kutokana na hitilafu
hiyo, mafundi walitengeneza na
kurejesha umeme katika hali
yake ya kawaida saa 6:30 usiku
na tatizo hilo kwa sasa
limekwisha kutatuliwa na
maeneo yote yana umeme
isipokuwa wale ambao wapo
katika mgawo ambao ratiba yake
ilishatangazwa.
“Uongozi wa shirika unaomba
radhi kwa hitilafu hiyo ya umeme
iliyotokea jana (juzi) ambapo
maeneo mengi yalikosa umeme
hususan kuleta usumbufu
mkubwa kwa mashabiki wa
mpira na wadau wengine,”
alisema Badra katika taarifa hiyo
ya Tanesco.

No comments:

Post a Comment