Sunday, July 17, 2011

viongozi 6 wa dini wakiri kujihusisha na dawa za kulevya

VIONGOZI sita wa madhehebu ya
dini wanaojihusisha na biashara
haramu ya dawa za kulevya
nchini, wamejitokeza mbele ya
Kamati ya Maadili ya Viongozi wa
Dini na Haki za Jamii na kukiri
kujihusisha na biashara hiyo kwa
muda mrefu sasa.
Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la
Polisi, baada ya kuhojiwa,
viongozi hao waliiomba Kamati
hiyo kutowataja hadharani
majina ama madhehebu yao kwa
kuhofia kubezwa kwa
madhehebu wanayoyaongoza.
Akizungumza mwishoni mwa
ziara yao Zanzibar, Mwenyekiti
wa Kamati hiyo, Mchungaji
William Mwamalanga wa Kanisa
la Pentekoste Tanzania, alisema
mbali ya orodha hiyo, ipo pia ya
watu 18 wakiwemo
wafanyabiashara wakubwa na
wanasiasa wanaojihusisha na
biashara hiyo.
Alisema orodha zote zitafikishwa
kwa Mkuu wa Kitengo cha Polisi
cha Kupambana na Dawa za
Kulevya nchini.
Mchungaji Mwamalanga alisema
tatizo la ongezeko la dawa za
kulevya, pia inazihusu nchi
mbalimbali duniani na kwamba
kamati hiyo itakutana na kamati
nyingine kama hizo za nchi za
Maziwa Makuu kuzungumzia
ufumbuzi wa suala hilo.
Alisema mkutano huo pia
utapendekeza kwa mabunge ya
nchi hizo na Bunge la Afrika
Mashariki kutunga sheria za
kuwafilisi wote waliojilimbikizia
mali kutokana na biashara za
dawa za kulevya kwa nchi
wanachama.
Hata hivyo, Kamati hiyo ya Maadili
ya Viongozi wa Dini na Haki za
Jamii ikiwa Visiwani, imesifu na
kupongeza juhudi za Jeshi la
Polisi kwa hatua zao za
kukabiliana na ongezeko la dawa
za kulevya.
Akizungumzia kero ya dawa za
kulevya visiwani hapa, Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Mjini
Magharibi, Aziz Juma Mohammed,
alisema Jeshi hilo limekuwa
likiwakamata wengi wa
wafanyabiashara na watumiaji
wa dawa za kulevya na
kuwafikisha mahakamani.
Hata hivyo, Kamanda Aziz alitoa
mwito kwa wananchi na wadau
mbalimbali wa usalama
kuendelea kusaidiana na Jeshi
hilo kwa kutoa taarifa za wale
wote wanaojihusisha na
mtandao wa dawa hizo.
Kamanda Aziz alisema kama kila
mwananchi atatoa taarifa za siri
Polisi za kuwepo kwa mtu ama
kundi la watu wanaojihusisha na
biashara hiyo ama uhalifu
mwingine wowote, ni wazi kuwa
Polisi itawatia mbaroni.
Wiki iliyopita, watu wawili
wakazi wa Dar es Salaam,
wamekamatwa kwenye Uwanja
wa Ndege wa Kimataifa wa
Abeid Amaan Karume, Zanzibar
kwa nyakati tofauti wakitokea
Brazil, ambapo kila mmoja
alipatikana na kiasi kikubwa cha
dawa za kulevya aina ya kokeini.

No comments:

Post a Comment